Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa, inapanga kuwaondoa raia wake huku nchini Afrika Kusini baada ya kushadidi hujuma na mashambulio dhidi ya raia wa kigeni katika nchi hiyo.
Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini umesema umeanza zoezi la kuwatambua Watanzania waishio katika maeneo ya hatari nchini humo kabla ya kuanza hatua za kuwaondoa na kuwarejesha nyumbani.
Mkuu wa Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mindi Kasiga, amesema kwamba Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini umepeleka maofisa wake katika mji wa Durban kuangalia hali ilivyo.
Kasiga ameongeza kuwa, serikali imeshatoa mwongozo wa namna ya kuwaondoa raia wake nchini Afrika Kusini.
Aidha amesema, utaratibu wa kuwaondoa Watanzania upo tayari, lakini si kila Mtanzania anayeishi Afrika Kusini ataondolewa, bali wale walio katika maeneo hatari.
Mamia ya raia wa kigeni wanaoishi Afrika Kusini wamekimbilia katika kambi zilizowekwa katika miji ya Johannesburg na Durban wakihofia maisha yao na hadi sasa raia sita wa kigeni wameshauawa katika hujuma hiyo.
Mashambulizi hayo yalishika kasi zaidi baada ya Mfalme wa Zulu, Goodwill Zwelithini kaBhekuzulu, kunukuliwa na vyombo vya habari mwezi uliopita akisema kuwa raia wa nchi za Kigeni wanapaswa kuondoka nchini humo.
No comments:
Post a Comment
Note: only a member of this blog may post a comment.